144,000 NI NANI?



Katika Kitabu cha ufunuo wa Yohana Sura ya saba tunaona kuwa kuna watu ambao idadi yake ni 144000 ambao hao ndio washindi wa dhambi kipindi Yesu anakuja tena kwa mara ya pili. Kwa vile watu hawa ambao wamefua mavazi yao na kujiweka tayari na ambao wanatabia ya Kristo katika mienendo yao ya maisha na kweli walioipokea ndio wanayoiishi kabla ya kuja kwake Yesu. Tunajua kuwa Watu hawa 144,000 wanatoka katika wakati huu ambao tuliopo. Katika wakati tuliopo kutakuwa na aina mbili ya waadventista wasabato ambao ni wa Kanisa la Fildefia na wa kanisa la Laodekia. Wa kanisa la Fildefia ndio kanisa la Mungu ambao wanajulikana kama pia ni 144,000 ambao watatiwa Muhuri. Lakini kwa upande mwingine wa kanisa la Laodekia ni waadventista wasabato ambao wanajua ukweli lakini hawaendi sawa sawa na huo ukweli wakijiona kuwa hawana haja na kitu.
Nikasikia hesabu yao waliotiwa muhuri katika kila kabila ya Waisraeli, watu mia na arobaini na nne elfu (Ufunuo 7:4)

Tunaona kuwa watu hawa ndio ambao watatiwa Muhuri wa Mungu katika paji la nyuso zao. Sasa kwa vile kanisa la waadventista wasabato lipo katika Hali ya Laodekia na uwepo wa Mungu haupo ndani yake,

Kanisa lipo katika hali ya Laodekia. Uwepo wa Mungu haupo katikati yake. (EGW, Last day Events, 49.1)
Inamaana kuwa watu hawa Hawatoki katika kanisa la Laodekia bali wanatoka katika kanisa la Filedefia.Hawa ni watu kutoka katika kanisa la Fildefia. Hili ndilo kanisa la kweli la Mungu katika kipindi hichi cha siku za Mwisho. James White alisema kuwa kanisa la filedefia lilianza mwaka 1844 ambao walikuwa ni watu wanaoangalia maandiko na kutafuta nuru ya Kristo na watakuwepo mpaka Yesu atakaporudi tena.  Yoyote ambaye anaishi sawa na neno la Yesu na sheria zake na kuakisi tabia ya Kristo ya upole na upendo anaahadi kuwa atatiwa muhuri nakuwa miongoni mwa hawa 144,000

Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye. Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina languTazama, nakupa walio wa sinagogi la Shetani, wasemao kwamba ni Wayahudi, nao sio, bali wasema uongo. Tazama, nitawafanya waje kusujudu mbele ya miguu yako, na kujua ya kuwa nimekupenda. Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi. Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako. Yeye ashindaye, nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo tena kabisa, nami nitaandika juu yake jina la Mungu wangu, na jina la mji wa Mungu wangu, huo Yerusalemu mpya, ushukao kutoka mbinguni kwa Mungu wangu, na jina langu mwenyewe, lile jipya. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. (Ufunuo 3:7-13)
Tunagundua kitu hapa kuwa Kanisa la Filadelfia ni kanisa ambalo watu wake ni waaminifu kwa Mungu na wametunza neno la Mungu. Kwa vile Biblia imesema kuwa "utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi" Tunajua kuwa kanisa hili lipo mpaka sasa na ni watu ambao watashikilia imani yao kipindi cha majaribu. Watu wa Mungu ambao watatetea imani zao mpaka kufa ndio watu wa kanisa la Filadelfia. Kwa maana  hiyo watashinda majaribu ya shetani katika kipindi hicho cha kujaribiwa ambacho muda sio mrefu kina kuja, watatiwa muhuri wa Mungu kuwa ni washindi wa Dhambi. Ellen White alisema

“Unafikiri kuwa wale wanaoabudu katika miguu ya watakatifu (Ufunuo 3:9) mwishoni wataokolewa. Hapa lazima nitofautiane na wewe, Kwa kuwa Mungu amenionesha kuwa hawa ni kundi la wanaojiita waadventista ambao wameasi na wamemsurubisha mwana wa Mungu upya, na kumuweka katika aibu ya wazi. Na katika saa ya majaribu ambayo itakuja, kuonesha tabia halisi ya kila mtu, watajua kuwa wamepotea milele na watajawa na sononeko rohoni, na watainama katika miguu ya watakatifu” (EGW, A word to the little Flock, p.g 12)

Tunaona kuwa Ellen White anasema wale ambao wataabudu katika miguu ya watakatifu ni waadventista pia, lakini waadventista hawa ni wale ambao wameasi kwa kutoenda sawa sawa na kweli ambazo Mungu ametoa. Hivyo tunaelewa kuwa katika kanisa la waadventista wasabato kuna waadvetista wa kweli ambao ndio Kanisa la Filedelfia na kuna kundi la wasabato wa uongo ambao ndio sinagogi la Shetani au kwa jina lingine ni kanisa Laodekia lakini wapo humo humo kanisani wajiitao wayahudi kumbe sio wayahudi maana yake ni kwamba wanajiita ni waadventista wasabato lakini sio waadventista wasabato kweli. Sinagogi la shetani inaweza ikawa ni washiriki, viongozi wa kanisa, wachungaji, viongozi wa General conference n.k Lakini japokuwa na umaafuru wao na kuonekana kuwa ni watu wa Mungu lakini ukweli ni kwamba hawa ni sinagogi la shetani. Sasa Kwa vile Ellen White amesema kuwa Kanisa lipo katika hali ya Leodekia na uwepo wa Mungu haupo katikati yake tunaelewa kuwa Sinagogi la shetani katika Kanisa la Filedelfia ni waadventista wasabato ambao wanajua ukweli lakini hawaishi sawasawa na huo ukweli wanaojulikana tena kama kanisa Laodekia. 
Kuna ambao ni wasabato jina na kuna ambao ni wasabato wa kweli. Wasabato wa kweli ndio watu wa Mungu waliopo katika kanisa la Fildefia na wasabato walioasi kweli za Mungu ndio walio katika Kanisa la Laodekia ambao ni vuguvugu. Ellen White anasema

Hawa 144,000 wametiwa muhuri na wameungana kwa pamoja. Katika paji za nyuso zao wameandikwa jina la  Mungu, Yerusalem mpya na nyota yenye utukufu ambayo ina jina jipya la Yesu. Katika Furaha yetu na katika hali yetu ya utakatifu waovu walikasirishwa na wakafanya haraka Kunyanyua mikono yao ili watutupe gerezani, Tuliponyoosha mikono yetu kwa jina la Yesu wakaanguka wakiwa hawana msaada katika ardhi. Hivyo Sinagogi la Shetani walipoona kuwa Mungu anatupenda ambao tunaoshana miguu sisi kwa sisi na kusalimiana kwa busu takatifu, na wakaabudu katika miguu yetu (EGW, Early Writtings, p.g 15).
Tunaona kuwa hawa watu 144,000 ni watu katika kanisa la Filedelfia kwa maana sinagogi la Shetani limezungumziwa katika kanisa la Filedelfia. Hawa ndio ambao watatiwa Muhuri wa Mungu katika paji za nyuso zao. Sasa kwa vile Ellen White amesema kuwa sinagogi la shetani ni waadventista wasabato ambao hawaendeni sawa na neno la Mungu, Tunaelewa kuwa kuna wakati utafika ambapo waadventista wasabato watawasaliti waadventista wenzao. Kuwa ndani ya kanisa kuna wakati utafika ambapo waadventista walioasi kweli za Mungu watakapo watesa na kuwaweka gerezani waadventista wenzao ambao wanaamini na kushikilia katika kweli za Biblia. Na wakati huo umekwishaanza kwa maana wapo wengi ambao wanafutiwa ushirika kwa kuliambia kanisa la Laodekia makosa yake. Kwa hiyo mpaka sasa tumejifunza nini

i.                    Wanaojiita waadventista au waadventista wasioenda sawa na Nuru zilizofunuliwa sio waadventista kwa Mujibu wa Biblia.

ii.                  Fildelfia ndio kanisa la kweli la Mungu ambalo watu wa Mungu watapita katika saa ya Majaribu au pia inajulikana kama taabu ya Yakobo.

iii.                Wanaojiita waadventista au waadventista wasioenda sawa na kweli za Biblia hawa ndio sinagogi la shetani au kwa jina lingine ndio kanisa la Laodekia.

Ukweli ndio huu ya kuwa Mungu anakanisa lake. Kanisa lake sio jengo au dhehebu fulani bali kanisa la Yesu ni wale wanamuamini na kumuabudu Yesu katika kweli na Roho. Kuna wengi ambao wanajua kweli za Biblia lakini hawana upendo na hawana tabia ya Yesu. Kwa hiyo kila mmoja anatakiwa atambue kuwa kuwa mshiriki wa kanisa la waadventista msabato haimaanishi kuwa unauhakika wa kutiwa Muhuri au kuurithi ufalme wa mbinguni. Ellen White anasema
“Mungu anakanisa. Sio kanisa kubwa na wala sio kama taifa zima. Ni watu wanaompenda Mungu na kutunza amri zake. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao (Mathayo 18:20). Pale ambapo Yesu yupo pamoja na wachache ambao ni wanyenyekevu, hilo ndio kanisa la Yesu, Kwa maana uwepo wa juu wa yule mtakatifu anayeijaza milele, pekee unaweza kutengeneza kanisa” (EGW, The upward look, p.315)

Mungu anakanisa lake na kanisa lake sio hili linaloonekana kwa macho, bali ni lile kanisa ambalo limejengwa katika utii wa amri zake. Sisemi kuwa watu wasiwe wanahudhuria ibada kanisani kwasababu kanisa la Mungu sio Dhehebu la waadventista wasabato, ila ukweli ni kwamba, kanisa la Mungu ni wale wanaolitii jina la Bwana na kutunza na kuishi sawa sawa na Nuru zilizofunuliwa.  Kanisa la waadventista wasabato lenyewe linakiri kuwa ni kanisa Laodekia ambalo Mungu hayupo tena katikati yake.
Leo tunasita kusema kuwa sisi ni kanisa masalia, Bali ni Laodekia, Hao ndio sisi, sisi pekee yetu... Hakuna kikundi kingine cha kikristo kinaweza pingana au kusita kutambua hilo... Bila kupingika Kanisa la waadventista wasabato ndio kikundi kilichosemwa katika ujumbe wa siku za mwisho. (Adventist Review,  August 28,2008).

Kwa maana hiyo kanisa la waadentista wasabato linakiri kuwa ni Kanisa Laodekia. Hivyo sio kanisa aminifu kwa Mungu tena. Kuna watu wa Mungu ambao ni waaminifu na wanatunza imani ya waasisi wa kanisa. Kuna watu wa Mungu ndani ya kanisa na wasabato ambao watatiwa muhuri watu hawa ni watu kutoka kanisa la fildefia. Mungu anafanya kazi na mtu mmoja mmoja ndani ya kanisa la waadventista wasabato na sio tena kanisa kwa ujumla kama ilivyokuwa hapo mwanzo. Baada ya kuwa kanisa la waadventista wasabato kuwa katika uasi, Mungu hafanyi tena kazi na kanisa hili kama dhehebu bali uwepo wake utakuwa na wale wanaoakisi tabia ya Kristo katika maisha yao. Uwepo wa Mungu haupo katika dhehebu hili kwasababu tayari ni vuguvugu. Bali uwepo wa Mungu upo kwa mmoja mmoja. Yesu alisema.
Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.(Ufunuo 3:20).

Ujumbe huu wa Yesu upo katika kanisa la Laodekia katika kitabu cha ufunuo. Maana yake ni kwamba Yesu anaalika mtu mmoja mmoja kumkubali katika moyo wake na kuwa moto badala ya kuwa vuguvugu hata kama inamlazimu kupingana na kile kanisa inaamini. Yoyote ambaye atakubali kumfungulia Yesu moyo mwake, Yesu ataingia na kumgeuza moyo wake na kumpeleka katika Nuru za Biblia ambazo wakati mwingine zinapingana na kile ambacho kanisa linaamini kwa sasa. Watu hawa wa Mungu ndio watakuwa katika kanisa la Fildelfia ambalo ndio kanisa la Mungu ambalo linapewa Muhuri wa Mungu. Ndani ya kanisa la Wasabato kuwa watu wa Mungu na hao ndio kanisa la Mungu na sio Dhehebu la waadventista wasabato 

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA ALAMA YA MSALABA

MUNGU ANA NAFSI NGAPI?

1YOHANA 5:8 NA MATHAYO 28:19 ZINASEMAJE?