MUNGU ANA NAFSI NGAPI?


Ni wazi kuwa kila mmoja katika kanisa la Adventista wasabato na Wale ambao sio wasabato watajibu swali hili kuwa Mungu ana nafsi Tatu. Hii ni kutokana na Fundisho la Utatu mtakatifu. Nianze kwa eleza nini maana ya fundisho la utatu mtakatifu, Hili ni fundisho linalosema Mungu ni nafsi tatu yani Baba, mwana na Roho mtakatifu. Kwa maana nyingine ni  kwamba Mungu hawezi kuwa na nafsi moja bali siku zote ni tatu.  Lakini Swali la kujiuliza ni kwamba Je biblia Takatifu imesema Mungu ana nafsi tatu? Au ni mapokeo Kutoka katika kanisa Katoliki. Mwanafunzi yoyote mwenye nia ya kweli ya kujifunza pima hichi ninachokisema kama kimetokana na Biblia au hapana, kwa kutambua hilo basi inabidi tuangalie biblia kama jinsi inavyojifunua Yenyewe. Ni muda umefika ambapo inabidi tumwabudu Mungu aliyefunuliwa katika Biblia na sio Mungu aliyetengenezwa na kanisa Katoliki, muda umefika ambapo kanisa la wasabato linabidi liamshwe ili kuzingatia ujumbe wa malaika wa kwanza, ujumbe ambao kanisa la Mungu limeuweka pembeni au wenda hawajui unahusiana na nini. Lakini jambo moja tu ambalo ni wazi ni kwamba Mungu wa Mbinguni kwa kupitia maandiko yake huwa anajitetea na kujidhihirisha kuwa yeye ndiye Mungu wa Biblia. Tufunue Biblia Zetu tuangalie Biblia yenyewe inasemaje.
"Mkumbuke Ibrahimu na isaka na Israel watumishi wako ambao Uliwaapia KWA NAFSI YAKO na kuwaambia Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni. Tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele" (Kutoka 32:13).

Tukisema Mungu ana nafsi tatu tunapingana na Mstari huu unaoonesha wazi kuwa Mungu ana nafsi moja. Nafikiri kwa sisi tunaotumia kiswahili pale tunapotumia neno “kwa nafsi yako” kitu gani kinakuja akilini? Kwamba nafsi ni moja au zaidi ya moja? Ni wazi kuwa mstari umeonesha kuna nafsi moja. Tuone pia mstari mwingine unasemaje.
“akasema Nimeapa KWA NAFSI YANGU asema BWANA kwa kuwa umetenda neno hili wala hukunizuilia mwanao mwanao wa pekee. Katika kubariki nitakubariki na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni na kama mchanga ulioko pwani na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao"( Mwanzo 22: 13).

Ikiwa Tunafikiri kuwa Mungu ana nafsi tatu tujue kuwa Sio Mungu wa Biblia na  sio jinsi Mungu anavyojifunua Yeye mwenyewe maana katika mstari huu Mungu amesema wazi “kwa nafsi yangu” si dhani kuwa kuna mtu yoyote anayeweza tumia neno kwa nafsi yangu akimaanisha nafsi tatu. Maana kama ingekuwa ni tatu basi ingekuwa ni nafsi zetu. Kama Mungu angekuwa ni zaidi ya nafsi moja basi wingi ungetumika kuwa ameapa kwa nafsi zake. Lakini Mungu hasemi hilo, sasa sisi tunapata wapi hili jambo? Tuangalie mstari mwingine unasemaje.
"Bwana MUNGU ameapa KWA NAFSI YAKE asema BWANA Mungu wa majeshi Naizira Fahari ya yakobo, nachukizwa na majumba yake kwasababu hiyo nitautoa huo mji pamoja na wote waliomo ndani yake" (Amosi 6:8)

Hakika Mungu ni Mungu mwenye nafsi Moja. Katika yeye katika hakuna nafsi nyingine. Maana kama kungekuwa na zaidi ya nafsi moja angesema wazi kabisa. Lakini Mungu wetu ni Mungu anayependa kutufunulia ukweli wa biblia ili tupate kuwa huru. Mungu ameapa kwa nafsi yake, maana yake ni Kwamba yeye ni nafsi moja kama jinsi tulivyo mimi na wewe. Kama sisi tu nafsi moja, hata Mungu wetu naye ni hivyo hivyo maana tumeumbwa kwa mfano na sura yake. Tuendelee kuangalia Biblia inasemaje.
"BWANA wa majeshi ameapa KWA NAFSI YAKE akisema Hakika Nitakujaza watu kama Nzige nao watapiga kelele juu yako" (Yeremia 51: 14)

Ni wazi kuwa Mungu wa mbinguni ni Mungu mwenye nafsi Moja. Kwanini katika biblia kuwe na marudio ya neno moja tu kuwa ameapa kwa “nafsi yake” kama Mungu angekuwa ni nafsi tatu? Au je walioandika biblia walikosea katika uandishi wao? Hapana Bali yote yaliyoandikwa katika biblia ni pumzi ya Mungu. Ni Mungu mwenyewe anajidhihilisha wazi kuwa yeye ni mmoja tu. Mungu anashuhudia kuwa yeye ni nafsi moja kama jinsi mimi na wewe tulivyo na nafsi moja tu. Mungu anarudia mara kwa mara akionesha kuwa yeye ni nafsi moja tu wala hakuna mwingine.
"Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye mteule wangu, ambaye NAFSI YANGU imependezwa Naye nimetia roho YANGU juu yake naye atawatolea mataifa hukumu"(Isaya 42:1)

Mungu anaendelea kusisitiza kuwa ni nafsi moja tuu na sio tatu kama jinsi tulivyofundishwa. Katika hili ninaujasiri wa kusema hilo. Kwasababu Mungu mwenyewe anashuhudia hilo. Kama tuliweka mbali ushabiki wa kidini na wakimafundisho na kuanza kutazama vyema maandiko matakatifu utaona jinsi gani Mungu mwenyewe anajionesha kwetu. Kama Mungu angekuwa na nafsi zaidi ya moja basi asingesema kuwa nimeapa “kwa nafsi yangu”.  Tunaposema neno “Yangu” Je huwa tunamaanisha nafsi zaidi ya moja? Hapana lakini cha kushangaza ni kwamba tunapokuja kwa upande wa Mungu basi akili zetu zinapumbazwa na fundisho ambalo halipo katika biblia. Tuendelee kuangalia  
MIMI BWANA nimekuita katika haki nami nitakushika mkono na kukulinda na kukutoa uwe agano la watu na nuru ya mataifa"( Isaya 42: 6)

Sidhani mpaka Mungu aseme neno “Mimi” bado tu amaanishe nafsi zipo tatu. Ndugu zangu katika Bwana tuache biblia ijitetee, tuache biblia ijitafsiri. Tuchunguze kile tunachofundishwa kanisani kama kweli kimetokana na Biblia. Tuache Mungu mwenyewe aseme kuwa yeye ni nafsi moja au tatu. Ndugu zangu tusifanye mioyo yetu kuwa migumu kiasi cha kubishia mpaka Mungu mwenyewe aliyejifunua kwetu sisi. Je Kuna Mungu mwingine? Tuone jinsi gani Mungu wetu anachosema

"Fahamu sasa ya kuwa MIMI naam MIMI NDIYE wala hapana MUNGU MWINGINE ila MIMI. Naua MIMI, nahuisha MIMI. Nimejeruhi tena naponya wala hapana awezaye kuokoa katika mkono WANGU. ( Kumb 32: 39)

Wewe msomaji ni shahidi jinsi Mungu anavyojifunua. Unaona wazi jinsi gani neno lake ni lipo wazi kuwa yeye Mungu ni nafsi moja tu. Kama Mungu angekuwa zaidi ya nafsi moja, sasa kwanini aseme neno “Mimi” badala ya “sisi”. Hili tu liache likikuumiza akili kufikiria. Hili tu likufanye utafakari kile ulichokuwa unakijua kuhusu Mungu. Kwani je Neno linalotoka kwa Mungu si neno la kweli? Au je kuna kosa gani lililopo katika Biblia takatifu ya Mungu? Sasa kama hakuna kosa lolote kwanini tunaendelea kuamini kuwa Mungu ni nafsi tatu wakati Mungu mwenyewe amesema wazi kuwa yeye ni nafsi moja tu? Bila Shaka hakuna Mungu mwingine ila yeye. Mungu mmoja mwenye nafsi moja.

"MIMI NI BWANA wala Hapana mwingine zaidi yangu MIMI hapana Mungu, nitakufunga mshipi ijapokuwa hukunijua"( Isaya 45: 5)

Tazama jinsi Mungu anavyorudia kuelezea. Tazama Mungu ambavyo hachoki kusisitiza kuwa yeye ni mmoja tu na sio watatu. Tazama Jinsi Mungu anavyoendelea kutoa maelezo kuwa bila yeye hakuna mwingine. Kwa jinsi gani Mungu anatupenda kiasi cha kwamba hataki atuache gizani katika mafundisho  la uongo kutoka kanisa katoliki.  Eeh Mungu endelea Kuzungumza na wale wanaosema wewe ni Nafsi tatu.
Lakini MIMI NI BWANA Mungu wako tangu nchi ya Misri wala hutamjua mungu mwingine ila MIMI wala zaidi ya MIMI hakuna mwokozi" (Hosea 13: 4)

Mungu mwenye nafsi moja huyo ndiye Mungu wa kweli. Yoyote anayesoma Neno la Mungu katika uaminifu wa Moyo ataweza kugundua kuwa Biblia huwa haijipingi. Biblia imesema wazi kuwa Mungu wetu Mungu wa mbingu na nchi ni Mungu mmoja mwenye nafsi moja tu. Kama angekuwa ni zaidi ya moja basi Mungu wetu angetueleza wazi. Lakini katika maandiko yake matakatifu Mungu amejifunua kwetu ili tupate kuwa huru kutoka katika mafundisho yanayo mvunjia heshima maana hakuna mnyama wala binadamu aliye na nafsi tatu.

"Bali BWANA ndiye Mungu wa Kweli. Ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele, Mbele za ghadhabu YAKE nchi yatetemeka. Wala mataifa hawawezi kustahimili hasira YAKE" ( Yeremia 10:10)
Baada ya kuona Jinsi biblia inavyojieleza na kujibu swali Kwamba Mungu ni mwenye Nafsi Moja na Biblia inamtaja Kuwa ni Mungu pekee tuangalie katika Vitabu vya agano jipya Vinasemaje. Je Mungu aliyefunuliwa katika vitabu vinavyojulikana kama vitabu vya agano la kale ni tofauti na Mungu aliye katika vitabu vya agano jipya. Au je Mungu katika agano jipya ni Mungu mwenye nafsi tatu lakini katika agano la kale ni Mungu mwenye nafsi moja? Ili tupate majibu ya maswali yetu tuendelee kuangalia nini ambacho biblia inasema.

"Twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu Kristo siku zote tukiwaombea"(wakolosai 1:3)
Mtume paulo anasema wazi kuwa Mungu ni mmoja ambaye ndiye Baba wa bwana wetu Yesu Kristo. Nafikiri hakuna mstari katika biblia ulio wazi kama huu. Mstari umeweka bayana kuwa Mungu ni baba yake Yesu Kristo. Yesu ana baba mmoja tu, na huyo baba ndiye Mungu. Yule Mungu aliyeapa kwa nafsi yake katika agano la kale. Ndiye yule Mungu aliyesema hakuna “Mungu mwingine ila mimi” katika agano la kale.

"Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo aliyetubariki kwa baraka  zote za rohoni katika ulimwengu wa roho ndani yake Kristo"( Waefeso 1: 3)
Mtume Paulo anaendelea sisitiza  kwako kuwa Mungu si nafsi tatu Kuwa Mungu ni mmoja aliye baba wa Bwana Yesu. Baba ni mmoja hivyo Mungu ni mmoja. Hakuna neno wazi kama hili. Mungu amejidhihilisha mara nyingi akishuhudia kuwa yeye ni nafsi moja tu. Mtume Paulo hakufundisha kuwa Mungu ni zaidi ya nafsi moja. Bali alisema wazi kuwa Mungu ni mmoja aliye baba wa Mwana wa Mungu Yesu Kristo.

"Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa Rehema, Mungu wa faraja yote"(2wakoritho 1:3)

Mtume Paulo anaendelea tukoa msisitizo kwako kuwa Mungu ni nafsi tatu kwamba sio hivyo ila Mungu ni nafsi moja Naye ndiye Baba wa wa Bwana wetu Yesu Kristo. Mungu wetu huwezi nyamaza kimya kama kuna uongo unaoonekana kulibeba kanisa. Paulo ameweka bayana kuwa Baba pekee ndiye Mungu mmoja zaidi ya hapo Paulo mtume wa Mungu hakusema chochote.
Lakini kwetu sisi MUNGU NI MMOJA TU, ALIYE BABA ambaye vitu vyote vimetoka kwake nasi tunaishi kwake, yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo na sisi kwa yeye huyo"(1 Wakorintho 8:6)

Msomaji ni shahidi kuwa mstari huu umejikamilisha. Na kubaliana sawa sawa na kile kilichoelezwa katika agano la kale. Hakuna ukweli kama huu ya kuwa Mungu ni Baba, na Baba ndiye Mungu. Yeye ndiye aliyesema hakuna mwingine ila yeye. Yesu Naye anasema Hili.
"Yesu akamwambia usinishike kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba, Lakini enenda kwa Ndugu zangu ukawaambie Ninapaa Kwenda kwa BABA YANGU NAYE NI BABA YENU, KWA MUNGU WANGU NAYE NI MUNGU WENU" (Yohana 20:17).
Yesu anaweka wazi kuwa Baba yake ndiye Mungu wetu Baba Mmoja mwenye nafsi moja ndiye Mungu wetu, Yesu  anaongea na wewe Kuwa yeye daima ni Nafsi moja tu. Yesu naye ana Mungu wake ambaye ndiye Baba. Yesu amesema wazi kuwa baba yake ndiye Mungu wa mbingu na nchi.

"Na uzima wa Milele ndio huu wakujue wewe MUNGU WA PEKEE WA KWELI  na Yesu kristo uliyemtuma" (Yohana 17:3)
Mjue Mungu wa kweli upate uzima wa milele, usifanye moyo wako kuwa mgumu, mwabudu Mungu mwenye nafsi moja ambaye ni Baba, tambua kuanzia sasa kwamba Kuna Baba mmoja huyo Baba ndiye Mungu wa kweli. Wakati umefika tumwabudu Mungu aliye kwenye Biblia na sio Mungu wa kutengenezwa na Mistari michache ya Biblia iliyotafsiriwa vibaya tuangalie na kuijadili Mistari hii michache iliyopotoshwa ili kuonekana kuwa ina thibitisha utatu katika sura ifuatayo. Tumwabudu Baba yeye ndiye Mungu wa Kweli ndani yake hakuna Nafsi nyingine ila Yeye pekee yake. Wenda msomaji anaweza kujiuliza vipi kuhusu ule mstari unaosema wapo watatu washuhudiao mbinguni Baba neno na Roho na hawa ni umoja (1yohana 5:8) na ule wa Kwa jina la Baba na mwana na Roho mtakatifu (Mathayo 28:19). usikose kusoma post inayofata imeeleza wazi kabisa kuhusu mistari hii ambayo kwa mara nyingi huwa inatumika kufundisha kuwa Mungu ni utatu.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA ALAMA YA MSALABA

1YOHANA 5:8 NA MATHAYO 28:19 ZINASEMAJE?