1YOHANA 5:8 NA MATHAYO 28:19 ZINASEMAJE?



1.     1YOHANA 5:8

"Kwa maana wako watatu washuhudiao Mbinguni Baba na neno na roho mtakatifu na watatu hawa ni umoja"(1yohana 5:8)

Kwa kuanza kabisa, mstari huu ni mstari maarufu sana na unatumiwa kama ndio mstari mkuu unaoonesha kuthibitisha kuwa Mungu ni nafsi tatu. Lakini kwa mtu yoyote yule ambaye ni mwaminifu wa moyo na moyo wake hauna mabishano atajiuliza kwanini katika Mistari mingi ya Biblia Mungu mwenyewe anashuhudia kuwa yeye ni nafsi moja afu mstari mmoja huu ndio ubadili maana nzima ya Mungu mwenyewe? Na kuna watu japokuwa umetoa mistari mingi ya biblia kuonesha kuwa Mungu ni mmoja lakini bado anatumia mstari huu kutokukubali ukweli wa biblia hata kuifumbia macho mistari ya wazi inayoonesha kuwa Mungu ni nafsi moja tu. Sasa taratibu na tuangalie mstari huu kwa kina. Katika mstari huu msomaji na angalie vizuri. Je katika mstari huu wapi panaposema Mungu ni nafsi tatu? Au wapi panaposema kuwa Baba, mwana na Roho ni nafsi tatu za Mungu? Hata wewe msomaji unaona wazi kuwa Mstari hausemi chochote kuhusu Mungu kuwa na Nafsi tatu. Sasa kama mstari hausemi Mungu ananafsi tatu kwa nini tudhani  Mungu ni nafsi tatu? Mstari umesema wazi Kuwa Baba mwana na Roho ni umoja. Na umoja wao ni katika ushuhuda ule wanaotoa. Hichi ndicho mstari huu unasema. Tujiulize Nini maana ya neno umoja? Je watu wakiwa na umoja wanaungana na kuwa kiumbe chenye nafsi nyingi au wanakuwa katika hali ya kupatana na kunia mamoja?  kwa mfano, umoja wa watu watatu unawafanya waungane na kuwa mtu mmoja katika nafsi tatu? Je ikiwa mimi wewe na yule tunaumoja, Je miili yetu inaungana na kuwa mwili mmoja wenye nafsi tatu? Sasa kwanini nauliza haya maswali? Ni ili tuweze kutafakari nini maana ya umoja kwa maana ile ile tunayotumia katika mazingira ya kila siku. Tuangalie mfano

"Kwa hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe nao watakuwa mwili mmoja"(Mwanzo 2:24)
Katika ndoa Je mwanaume na mwanamke wanaungana na Kuwa Mwili mmoja wenye nafsi mbili? Hapana. Bali umoja wao ni katika kupendana, kutunzana, Na kunia mamoja lakini kamwe hawawezi kuungana na Kuwa mwili mmoja mwenye nafsi mbili. Hata msomaji ni shahidi kuwa hakuna ndoa inayowafanya wanandoa waungane na kuwa Mtu mmoja katika nafsi mbili. Tuangalie mfano mwingine

“Wote wawe na umoja kama wewe Baba ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.”(Yohana 17:21)

Yesu aliwaombea wanafunzi wake kumi na mbili wawe na umoja kama jinsi yeye Yesu na Baba yake walivyo na umoja hivyo umoja wa mitume ndio umoja ule ule kati ya Baba na mwana. Sasa tujiulize je umoja wa wanafunzi 12 wa Yesu unawafanya waungane na kuwa mtume mmoja katika nafsi 12?. Hapana kila mtume ni nafsi huru. Sasa Yesu aliposema umoja alikuwa anamaana umoja wa aina gani?

Hata na sisi sote tutakapoufikia Umoja wa imani na kumfahamu sana mwana wa Mungu, hata kuwa mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo (Waefeso 4:13)

Yesu alikuwa anawaombea wanafunzi wake wawe na umoja wa imani. Katika kumuamini Yesu Kristo.Watu waliokatika kanisa moja wanaumoja katika Imani, Umoja wao hauwafanyi wawe mwili mmoja katika nafsi nyingi. Lakini kitu cha kushangaza ni kwamba unapokuja katika umoja wa Baba na Mwana na Roho watu wanaanza kumaanisha kuwa hawa watatu wanaungana na kuwa nafsi tatu kitu ambacho hata biblia haisemi kuwa Mungu ni nafsi tatu wala hakuna wanafunzi wa Yesu walioungana na kuwa Mtume mmoja katika nafsi 12. Tunajua kuwa umoja wa Wanafunzi wa Yesu ndio umoja kati ya Baba na Mwana, lakini kwa upande wa wanafunzi wa Yesu, umoja wao hauwafanyi waungane na kuwa mtume mmoja katika nafsi 12, lakini kwa upande wa Baba mwana na Roho umoja huo unawafanya waungane na kuwa mmoja katika nafsi tatu jambo ambalo linashangaza sana. Tunasahau kuwa umoja wao ni katika ushuhuda. Kama imetokea ajali walioshuhudia ile ajali wanatoa maelezo mamoja ushuhuda huu unawafanya wawe ni umoja . Je ushuhuda wa watu walioona ajali fulani unawafanya wawe mwili mmoja katika nyingi? Hapana kila mmoja ni Nafsi inayojitegemea na hakuna muunganiko wowote. Sasa Mungu mwenyewe amesema yeye ni Nafsi ngapi?

"Akasema Nimeapa kwa NAFSI YANGU asema BWANA kwa kuwa umetenda neno hili wala hukunizuilia mwanao mwanao wa pekee"( Mwanzo 22:16)

kama Mungu angekuwa ni zaidi ya nafsi moja kwanini anasema Nimeapa kwa "NAFSI YANGU" au je neno hili huwa linatumika pale ambapo nafsi zinakuwa nyingi? Kama Mungu angekuwa ni zaidi ya nafsi moja Basi angesema Ameapa kwa Nafsi "ZAKE"  lakini hapana Mungu anashuhudia kuwa Yeye ni nafsi moja tu. Mstari mwingine

"Tazama mtumishi WANGU nimemtegemezaye mteule WANGU ambaye NAFSI YANGU imependezwa naye nimetia roho YANGU juu yake naye atawatolea mataifa hukumu"( isaya 42:1).

Tazama jinsi Mungu mwenyewe anavyojishuhudia kuwa yeye Ni nafsi Moja tu. Sasa kati ya watatu hawa  washuhudiao mbinguni nani ni Mungu?

"Na ahimidiwe Mungu, Baba Wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema Mungu wa Faraja yote"( 2wakorintho 1:3)

Sasa tunaelewa kuwa Umoja wa Baba na Mwana na Roho katika mstari huu hauwafanyi waungane na kuwa mmoja katika nafsi tatu, bali umoja wao ni katika Ushuhuda wanao utoa, Ushuhuda wa Baba ni sawa na ushuhuda wa Mwana na ushuhuda wa Mwana ni sawa na ushuhuda wa Roho na ushuhuda wa Roho ni ushuhuda wa Baba na mwana. Hii ndio maana halisi ya umoja. Hivyo basi japokuwa Baba Mwana na Roho ni Umoja katika ushuhuda, Baba ndiye Mungu ambaye Biblia imemtaja.

Kwa upande mwingine mstari huu haukuwepo katika maandiko halisi ya Mtume Yohana maneno hayo yaliingizwa baadae ili kuunga mkono fundisho la utatu. SDA bible commentary imesema kuwa,

Kifungu hiki kama kinavyoonekana katika KJV hakipo katika nakala yoyote ya kigiriki kabla ya karne ya 15 na 16. Maneno haya yasiyokubalika yalipata njia kuingia katika KJV kwa kupitia Maandiko ya Kigiriki ya Erasmus (Ona Vol. V p.141). Inasemekana kuwa Erasmus alitaka kuingiza maneno haya yasiyokubalika katika Maandiko yake kama angeoneshwa hata nakala moja inayoonesha kuwepo na maneno hayo. Maktaba ya Dublin imetengeneza Nakala kama hiyo (Inajulikana kama 34) na Erasmus aliingiza kifungu hicho katika maandiko yake. Sasa inaaminika kuwa matoleo ya baadaye ya Vulgati yalipata kifungu hiki kwa makosa ya mwandishi aliyeyaingiza kimakosa  katika maandiko ya biblia ambayo alikuwa ananakiri. Maneno haya yasiyokubalika yamekuwa yakitumika sana katika kuunga mkono fundisho la utatu, lakini katika kuangalia ushahidi wa kushtusha unaopinga uhalali wake, kukubalika kwake umekuwa ni kiasi kidogo na huwa hayatumiki. Japokuwa yanaonekana katika Vulgati tafsiri ya kikatoliki kuhusu Maandiko matakatifu ni wazi inakubali kuhusu maneno hayo “sasa inaaminika kwamba kifungu hichi ambacho sasa kinaitwa Comma Johanneum iliingia katika maandiko ya kale ya kilatini na Vulgati, Yalipata upenyo kuingia katika maandiko ya kigiriki katika karne ya 15 na 16 (SDA Bible Commentary vol. 7 675)

Ni wazi kuwa maneno hayo yaliingizwa katika Biblia lakini hayakuwa ni maneno halisi yaliyoandikwa na mtume Yohana, maneno haya yaliingia ili kuunga mkono Fundisho la utatu ambalo halina misingi yoyote kutoka katika maandiko. Ili kwamba ionekane kuwa fundisho hili ni la Biblia waliingiza maneno hayo ili kuonesha kuwa fundisho hili lipo katika bibia.

2.     MATHAYO 28:19.

“Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi mkiwabatiza kwa jina la Baba na mwana na Roho mtakatifu”(Mathayo 28:19)

Kila mmoja ni mwanafunzi wa Kristo kama Kristo anaishi ndani yetu. Kama roho wa kristo anaishi ndani yetu, basi sisi tu wanafunzi wa Kristo. Kristo anawaambia wanafunzi wake kuwa enendeni duniani kote kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wake. Kila mmoja anajukumu la kuleta watu kwa Kristo. Kila mmoja ana kazi ya kufanya kuhakikisha wanaokombolewa ni wengi. Sasa mstari unasema kuwa, hawa wanafunzi wabatize kwa jina la Baba la mwana na la Roho mtakatifu. Kila mmoja anayefika hapa inabidi awe makini sana ili kuona maana halisi inayozungumziwa hapa. Mara nyingi wanafunzi wa Biblia wanapofika hapa wanasoma huu mstari kama vile unathibitisha kuwepo kwa utatu.

Sasa tuangalie kwa umakini huu mstari na tuone je unathibitisha kuwepo kwa utatu au la? Kwanza kabisa msomaji arudie kusoma tena huu mstari. Baada ya kusoma tena huu mstari msomaji na ajiulie je katika mstari huu, ni wapi panaposema kuwa Baba, mwana na Roho mtakatifu ni nafsi za Mungu? Au ni wapi panaposema kuwa Baba mwana na Roho wanaunda Mungu mmoja? Mstari hausemi kabisa hayo lakini mara nyingi tunaposoma Biblia tunakuwa na maana yetu kichwani ambayo sio sahihi. Mstari huu umesema wazi kuwa mataifa wakabatizwe kwa jina la Baba na Mwana na Roho mtakatifu, hausemi hata kidogo kuwa “Mungu ana nafsi tatu”. Hata msomaji ni shahidi kuwa mstari hausemi kuwa Mungu ni nafsi tatu. Sasa kama mstari hausemi kuwa Mungu ni nafsi tatu. Kwanini sisi leo hii tunautumia kama ndio mstari mkuu unaothibitisha kuwa Mungu ana nafsi tatu wakati mstari wenyewe hausemi hilo? Mstari huu umetafsiriwa Vibaya na wengi, na wengi hawajui jinsi gani mstari huu umetafsiriwa kuthibisha kitu ambacho hakipo katika Biblia. Hivyo kwa ufupi kabisa msomaji ni shahidi kuwa mstari hausemi kuwa Mungu ni nafsi tatu, wala hausemi kuwa Baba,mwana na Roho wanashirikiana kuunda Mungu mmoja mwenye nafsi tatu.

Pia mstari umesema kuwa Ubatizo ni kwa jina la Baba na Mwana na Roho mtakatifu tulinganishe na mistari mingine katika Biblia

“Akaamuru wabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha” (Matendo 10:48)

Waliposikia Haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu” (Matendo 19:5)

Kwa maana  na bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu” (Matendo 8:16)

“Petro akawaambia Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu nanyi mtapokea kipawa cha Roho mtakatifu”( Matendo 2:38).

Katika Mistari hii tuliyosoma utagundua kuwa mitume walibatiza kwa jina la Kristo. Ubatizo ulikuwa kwa jina lake Yesu Kristo. Lakini tunaposoma Mathayo 28:19 tunaona kuwa ubatizo ni kwa jina la Baba na Mwana na Roho mtakatifu. Swali linaibuka je katika Ubatizo inabidi tubatizwe kwa jina la Yesu au kwa jina la Baba mwana na Roho mtakatifu? Ili tupate jibu zuri inabidi tuchuguze vizuri maandiko biblia inasema,

Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila Jina, ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe la vitu vya mbinguni na vya duniani na vya chini ya nchi na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA kwa utukufu wa Mungu Baba” (Wafilipi 2:9-10).

Ni wazi kuwa hakuna Jina lililo kuu kuliko Jina la Kristo. Hakuna jina ambalo limetukuzwa Mbinguni na duniani kuliko jina la Kristo. Jina la Yesu ndilo Jina kuu kuliko majina yote juu mbinguni na hata chini duniani hata chini ya dunia. Yesu Mwenyewe ana shuhudia kuwa

“Yesu akaja kwao akasema nao akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani”(Mathayo 28:18)

Yesu Kristo anashuhudia kuwa amepewa mamlaka Yote juu mbinguni na chini Duniani. Ni sahihi pia kusema kuwa Jina la Yesu ndio Jina lenye mamlaka yote juu mbinguni na chini duniani. Kwajina la Yesu kila jina litapiga goti na kukiri kuwa Yesu ni BWANA. Yesu alisema

Yesu akasema Mimi ndimi njia na kweli na uzima mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi (Yohana 14:6)

Kama hakuna mtu anaweza kwenda kwa Baba bila kupitia kwa Kristo ni sahihi kusema kuwa hakuna mtu yoyote ambaye anaweza kwenda kwa Baba bila Jina la Kristo. Bila jina la Kristo hakuna mtu ambaye anaweza kuokolewa. Jina la Kristo ndilo njia pekee ya mtu kuokolewa. Hivyo mistari hii imeweza kujibu swali letu kuwa ni Jina la Kristo tu ndilo Jina lililo bora kuliko majina mengine yale. Tunajifunza kuwa imempendeza Baba kuwa Jina la mwanae Yesu Kristo liwe jina kuu, kuliko majina mengine mbinguni hata kuliko Jina lake mwenyewe. Baba ameona Jina la mwana wake liwe jina zaidi hata lake huko juu mbinguni.

Sasa swali Jingine linaibuka kuwa kama Ubatizo unatakiwa kuwa kwa kupitia jina la Kristo kwanini Mathayo 28:19 imesema ubatizo ni kwa jina la baba na mwana na Roho mtakatifu? Na kwanini mstari huu usomeke tofauti na mistari mingine?

Ni kwa sababu kanisa katoliki lilibadili mstari huu wa biblia kutoka kusomeka kuwabatiza kwa jina la Yesu Kristo mpaka kusomeka kuwabatiza kwa jina la Baba na mwana na Roho mtakatifu. Ushahidi upo wazi kutoka katika kitabu cha kikatoliki cha Catholic Encyclopedia inasema

“Kanuni ya ubatizo ilibadilishwa kutoka kwa jina la Yesu Kristo kwenda kwenye maneno Baba mwana na Roho mtakatifu na kanisa Katoliki katika karne ya pili”(Catholic Encyclopedia book II p. 263)

Ni kanisa katoliki ndilo lililo badili mstari huu wa biblia ili kuingiza mstari ambao uonekane kuwa unathibitisha kuwepo kwa utatu mtakatifu. Lakini japokuwa wametumia njia hii ya udanganyifu, lakini bado mstari huu hauthibitishi kuwepo kwa Mungu mwenye nafsi tatu. Katika maandiko ya kale ya Eusebius anasema

“Katika neno moja na sauti alisema Nendeni na mfanye mataifa wanafunzi wangu kwa Jina langu wafundishe kuyashika yote niliyo waamuru” (Proof of the Gospel by Eusebius book III ch 6, 132 (a) p. 152)

Eusebius alikuwa ni mwana historia wa kikatoliki katika karne ya pili na ya tatu pia alikuwa ni Askofu  wa Kaesaria. Katika kitabu chake ananukuu mstari wa Mathayo 28:19 kutoka katika maandiko ya Kitabu cha mathayo halisi ambayo yaliandikwa kwa wino wake Mathayo. Katika Nukuu hiyo inaonesha jinsi gani ilivyo tofauti kabisa na jinsi Mstari huu unavyosomeka leo hii. Kanisa Katoliki lilibadili mstari huu ili kuufanya uonekane kuwa unaunga mkono uwepo wa nafsi tatu za Mungu. Yoyote asomaye huu mstari anatambua kuwa ni mstari ambao unapingana na mistari mingine ya Biblia ambayo imesema wazi kuwa Ubatizo ni kwa jina la Yesu na sio Jina la Baba mwana na Roho mtakatifu. Maneno haya Kwajina la Baba na la Mwana na la Roho mtakatifu ni neno linalotumiwa sana na kanisa katoliki katika sala. Kwa nini wanatumia sana haya maneno? Ni kwasababu kanisa lenyewe ndilo limeyaongeza maneno haya katika Biblia. Katekisim ya kanisa katoliki inasema

“Biblia inatuambia kuwa wakristo walibatizwa ndani ya Kristo (no.6). Ni mali ya Kristo. Matendo ya Mitume (2:38,8:16,10:48,19:5) inatuambia kuhusu kubatiza kwa jina la Yesu. Tafsiri nzuri ingekuwa ndani ya jina la Kristo. Ni katika karne ya nne tu kanuni ya Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho mtakatifu ikawa ni desturi” (Bible Catechism Rev, John C Kersten, S.V.D.., Catholic Book Publishing co, N.Y 1973 p. 164)

Katekism ya Kanisa Katoliki inatuambia kuwa ni karne ya nne kanuni ya kubatiza kwa jina la Baba na la Mwana na La Roho mtakatifu ikawa ni desturi. Inamaana kuwa yapokuwa badiliko la mstari wa Mathayo 28:19 lilifanyika katika karne ya pili lakini haikuwa ni desturi mpaka kufikia karne ya nne ndio ikawa ni desturi kubatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho mtakatifu. Ni wazi kuwa ilichukua muda sana mpaka jambo hili kukubalika maana mitume walibatiza kwa jina la Kristo wala sio kwa jina la Baba na la mwana na la Roho mtakatifu. Kardinali Rotzinger anasemaje

Msingi wa Msimamo wetu wa (Mathayo 28:19 utatu) wa Imani, ilichukua umbile katika kipindi cha karne ya pili na ya tatu kwa kushirikiana na sherehe ya ubatizo. Katika kuangalia asili, Maneno haya (Mathayo 28:19) yalitoka katika jiji la Roma” (Joseph Ratzinger-Pope Benedict XVI, Introduction to christianity 1968 p 82, 83)

Kardinali Joseph Ratzinger ambaye baadaye akaja kuwa Papa Benedict XVI anasema wazi kuwa maneno yaliyopo katika Mathayo 28:19 yalitoka katika jiji la Roma katika kipindi cha Karne ya pili na ya tatu. Kanisa Katoliki lenyewe linakiri kuwa maneno kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho mtakatifu yaliongezwa katika biblia na kanisa katoliki huko Roma. Maneno haya hayakuwepo kabisa katika Kitabu halisi cha Mathayo. Mwana historia Edmund Schlink anasema

“Amri ya ubatizo katika Mathayo 28:19 haiwezi kuwa ni historia halisi ya ubatizo wa Kikristo. Ni lazima angalau kuwa maneno haya yamebadilishwa katika umbo na kuongezwa na Kanisa katoliki” (Edmund Schlink The doctrine of Baptism p. 28,1972)

Mpaka kufikia hapa tumeweza kuelewa kwanini Mistari wa Mathayo 28:19 ni tofauti na mistari mingine inayohusiana na Ubatizo. Tumeweza kujifunza kuwa Biblia inatambua ubatizo kwa jina la Yesu Kristo na sio Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho mtakatifu. Kwa kweli Mungu hata siku moja hawezi kutuacha gizani bali anatoa ukweli ili tuweze tukawa huru. Kila msomaji na afahamu kuwa fundisho la utatu mtakatifu halina msingi wowote katika maandiko matakatifu wala hakuna sehemu yoyote ile ambayo utaona kuwa imeandikwa kuwa “Mungu ni nafsi tatu”. Wala hakuna sehemu hata moja ambayo utaona inasema Baba mwana na Roho ni nafsi tatu za Mungu. Wakati umefika kumwabudu Mungu anayefunuliwa ndani ya Biblia na sio Mungu aliyetengenezwa na Kanisa Katoliki. Watu wa Mungu wanamtambua Mungu aliyezifanya Mbingu na nchi na Kumwabudu Mungu aliye Mbinguni.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA ALAMA YA MSALABA

MUNGU ANA NAFSI NGAPI?