KANISA LA LAODEKIA


Kanisa la Laodekia ni kanisa la siku hizi za Mwisho. Ujumbe wa Kanisa la Laodekia unahusu wakristo wa kipindi chetu hasa wa kanisa la  waadventista wasabato. Mimi na wewe tunaweza tukawa ni miongoni mwa wale ambao Yesu amewaongelea katika kanisa la Laodekia. Hivyo kila mmoja na ajitafakari mienendo yake na kama inaendana na tabia ya kanisa la Laodekia inabidi aachane nayo haraka asije akatapikwa kutoka katika kinywa cha Yesu.


Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.   Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.  Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.  Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.  Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.  Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.  Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. (Ufunuo 3:14-22)


Tunaona kuwa hakuna sifa yoyote nzuri ambayo imetamkwa na Yesu kuhusu kanisa la Laodekia. Bali anasema kuwa ni kanisa ambalo sio moto wala sio baridi bali ni Vuguvugu. Tunajifunza nini hapa? kwa  Kawaida maji yaliyovuguvugu hapo mwanzo yalikuwa ya moto. Lakini kadiri muda unavyoendelea kwenda maji hayo yanaanza kupoa na kufikia wakati ambapo ni vuguvugu. Kwa maana hiyo kanisa la Laodekia hapo mwanzo lilikuwa ni kanisa ambalo limeshikilia kweli za Biblia. Lakini kadiri muda unavyoenda kanisa hili linaacha kweli zile za Biblia na kushikamana na Dunia. Mafundisho ambayo hayatokani na biblia au kutoishi sawa sawa na biblia ndio inafanya kuwepo na  uvuguvugu katika kanisa hili. Pale ambapo Kanisa linaacha kweli ya Biblia na kwenda katika njia zisizowekwa na Biblia, tunatambua kuwa kuna uvuguvugu ule ambao umesemwa katika kanisa la Leodekia.
Sasa Tunaona kuwa Yesu anasema kuwa kanisa hili atalitapika litoke katika mdomo wake. Maana yake ni kwamba kanisa hili Yesu ataliacha lisiwe kanisa lake kama halitatubu na ataondoa nafasi yake katika ufalme wa Mungu. Lakini swali linakuja Je kanisa hili la Leodekia linakubali makosa yake? Kitu cha ajabu ni kwamba kanisa hili linaona lenyewe halina mapungufu yoyote kwa maana linaona ni tajiri na limejitajirisha na wala halina shida na kitu chochote kile. Utajiri unaozungumziwa hapa ni utajiri wa mambo ya kiroho. Linajivunia utajiri wa kiroho, na kiburi chake kinaonekana wazi kwa maana Linasema halina haja na kitu. Maana yake ni kwamba Kama ni Biblia, linaona linaijua Biblia kiasi ambacho halina haja na kitu chochote kipya. Kama ni Kweli za Biblia, kanisa hili linaona Linajua kweli zote za Biblia kiasi ambacho halina haja na Kitu. Kama ni Kumjua Yesu, kanisa hili linaona linamjua Yesu mno kiasi cha kwamba halina haya na kitu chochote kile. Lakini Jinsi kanisa hili la Laodekia linavyojiona, ni tofauti kabisa na jinsi Yesu anavyoliona. Yesu akiliangalia kanisa hili anaona kuwa ni kanisa nyonge, lenye mashaka, na kipofu na lipo uchi. Japokuwa na mapungufu haja lakini kanisa Leodekia linaona kuwa ni tajiri na limejitajirisha mno. Kanisa Leodekia halitaki Kujifunza chochote kipya wala kuambiwa makosa yake. Hivyo kwa ufupi Tunaona wazi kuwa Kanisa la Laodekia hapo mwanzo lilikuwa ni kanisa Ambalo ni jema na lenye Ukweli mwingi wa Biblia likiwa limejiweka katika unyenyekevu na utayari wa kujifunza mambo mapya, lakini Limebadilika na kuwa ni kanisa lisilofaa kwa maana limegeuka na kuwa ni kanisa lililoasi likichanganya mafundisho ya ukweli na uongo na kuwa na kiburi cha kutotaka kusikia neno lolote jipya. Unabii huu wa kanisa la Laodekia unafanana sana na ule wa nabii Isaya.

"Mji huu uliokuwa mwaminifu umekuwaje kahaba! Yeye aliyejaa hukumu ya haki; haki ilikaa ndani yake, bali sasa wauaji!  Fedha yako imekuwa takataka, divai yako imechanganywa na maji.  Wakuu wako ni waasi, na rafiki za wevi; kila mtu hupenda rushwa, hufuata malipo; hawampatii yatima haki yake, wala maneno ya mjane hayawawasilii". (Isaya 1:21-23)

Mji mtakatifu unaosemwa na isaya ni kanisa la Mungu, na kanisa la siku hizi za Mwisho ni kanisa la Laodekia. Kwa maana hapo mwanzo kanisa Laodekia lilikuwa ni kanisa aminifu tena nyenyekevu lakini sasa limegeuka na kuwa ni kanisa ambalo limepotoka likichanganya mafundisho ya ukweli na uongo au kushindwa kuishi sawa sawa na Nuru zilizofunuliwa. Kutokana na hili, kanisa hili linatapikwa kutoka katika kinywa cha Yesu. Unabii wa kanisa Laodekia unalihusu kanisa la waadventista wasabato kwa kiwango kikubwa sana ambalo walipata nuru nyingi za Biblia na kuujua ukweli, lakini sasa haliishi sawa sawa na Nuru hizo ambazo Yesu alizitoa. Lakini sio rahisi Kanisa la Waadvetista wasabato kujiona lina makosa au kukubali kuwa msingi Fulani wa Kanisa au Miongozo na katiba ya Kanisa kuwa inamakosa kwasababu ya kiburi. Kwasababu linaamini kuwa limekamilika na halina makosa.Mara nyingi Kanisa linaona kuwa taratibu zake hazina makosa na kila mmoja ambaye ni mshiriki wa Kanisa la Waadventista wasabato atakubaliana na mimi kuwa ni mara nyingi sana tunaambiwa kuwa kanisa la wasabato ndio kanisa lenye kweli zote za biblia yaani ni kanisa lenye utajiri wa mambo ya kiroho, lakini ukweli huo hauna faida kama haubadili matendo yetu kumuakisi Yesu.Ellen White anasema

"Udunia hautakiwi uingizwe katika Kanisa, na kuoana na kanisa, na kufanya umoja nao. Kwa jinsi hii kanisa linakuwa limeasi kama jinsi ilivyoelezwa katika Ufunuo wa Yohana "Ngome ya kila ndege mchafu na mwenye kuchukiza"(Testimonies to Ministers, 265.1)

Ni kanisa gani Ellen White analisemea hapa? Ni kanisa la waadventista wasabato. Anaongea na wasabato waliondani ya kanisa. Pale ambapo Udunia unaanza kuingia katika kanisa, ni kiashiria kuwa uasi umeanza kuingia katika kanisa. Udunia unaonekana katika mavazi, Katika maongezi na katika mitindo mbalimbali ya maisha.  Kwahiyo  ndani ya kanisa la waadventista wasabato kama udunia umeingia katika kanisa maana yake ni kwamba ule uasi umengia na kufanya kanisa liwe katika uvuguvugu.

Kristo alipoona wayahudi kama taifa wameachana na Mungu, aliona pia Kanisa la Kristo linaungana na ulimwengu na upapa,  itambidi kusema na wale ambao walikuwa na nuru kubwa na maarifa mengi,kama alivyosema na wayahudi, " Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako"(EGW,Kress Collection 153.3)

Ni nani ambao walipewa nuru kubwa na maarifa mengi? Ni kanisa la waadventista wasabato. Katika Nukuu hii unaona kuwa Kama Kristo alivyoliacha Wayahudi waliomkataa ndiyo atakavyoliacha kanisa lake ambalo nalo limemuacha na kuongozana na Upapa na mambo ya dunia.Kama Kanisa linamuacha Kristo na kufatana na dunia na mafundisho ya upapa, Kristo hawezi kuwepo katika kanisa hilo. Makanisa ya kikristo yanaungana na upapa katika mafundisho. Kama Katika kanisa kuna mafundisho ya upapa ni wazi kuwa Yesu Kristo hawezi kukaa hapo mpaka kufanyike matengenezo ya kuachana na mafundisho hayo. Lakini kitu cha ajabu ni kwamba kanisa la Laodekia halioni kosa lake katika mafundisho yake. Kanisa la Laodekia Lina mkataa Kristo pamoja na haki yake kwa kushikilia mafundisho ya upapa. Tunaendelea kuona kuwa kadiri muda unavyoenda Kanisa la Waadventista wasabato linaendelea kulegeza misimamo yake katika mavazi, katika ibada, na katika kutengana na udunia na upapa. Japokuwa hili linaweza likaonekana ni sahihi mbele za wanadamu lakini halipo sawa mbele za Mungu.

Bwana Yesu ataendelea kuwa na watu wake aliowachagua kumtumikia. Wayahudi walipomkataaYesu, Mfalme wa uhai, aliuchukua ufalme wa Mungu utoke kwao na kuwapa watu wa mataifa. Mungu ataendelea kufanya kazi katika kanuni hii na kila tawi la kazi yake. Pale kanisa linapothibitishwa sio aminifu wenye neno la Bwana, bila kuangalia nafasi yao ilikuwaje, kuwa muito wao ni mkuu na mtukufu, Bwana hawezi tena kufanya kazi nao. Watu wengine watachaguliwa, kuchukua majikumu muhimu. (EGW, UL 131.3)

Je ni kanisa gani Ellen White analolimaanishia hapa? Hakuna kanisa lingine isipokuwa kanisa la Waadventista wasabato. Tunaona kuwa Yesu kristo anaangalia kwa kiasi gani kanisa ni aminifu katika Neno la Bwana. Kanisa la waadventista wasabato lilichaguliwa ili litangazie ulimwengu ujio wa Yesu mara ya pili. Yesu aliliinua na kulipa sabato kama ishara kati ya Mungu na kanisa lake. Lakini japokuwa nafasi yao ilikuwa ni kubwa na ya juu. Kwa vile limegeuka sasa na kuwa ni vuguvugu, tunajua kuwa uwepo wa Mungu haupo tena katika kanisa.

Wale ambao wanajisifu katika Nuru zao, na bado wanashindwa kutembea katika njia hiyo, Yesu anasema "Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu,[Kanisa la waadventista wasabato ambao walikuwa na nuru kubwa]  Ulitukuzwa hata mbinguni [Katika nafasi ya heshima] Utashushwa hata kuzimu: kama kazi iliyofanyika kwako ingelifanyika kwa Sodoma, ingelibakia mpaka hivi leo. (Review and Herald August 1, 1893) Maneno katika mabano yaliwekwa na Ellen White mwenyewe.

Tunaona kuwa Ellen White mwenyewe anasema wazi kuwa kanisa la waadventista wasabato ambao walipewa nuru kubwa linajisifu idadi ya Nuru walizo nazo lakini hawaendi sawa sawa na kweli hizo au nuru hizo, kuwa watashushwa hata kuzimu yani Yesu ataliacha kanisa lake la waadventista wasabato kwa maana linashindwa kutembea sawa sawa na Nuru hizo. Kanisa la waadventista wasabato linajisifu kuwa ndio kanisa pekee linalotunza sabato ya Kweli katika Biblia nani kweli kuwa sabato ni Jumamosi siku ya saba ya juma, Lakini linashindwa kwenda sawa na nuru zile ambazo Yesu alilipatia, kama jinsi sahihi ya kutunza sabato. Mpaka hapa tulipofika Ellen White anatusaidia kugundua kuwa Kanisa Leodekia linahusu Kanisa la waadventista wasabato kwa. Ambalo linajivunia Nuru walizonazo lakini hawaendi sawa na Nuru hizo.

Ujumbe kwa kanisa la Laodekia unahusu hali zetu. Jinsi gani ilivyowazi kwa wale wanaofikiri kuwa wanaukweli wote, wakiwa na kiburi katika maarifa ya neno la Mungu, wakati nguvu yake inayotakasa haipo katika maisha yao.Nguvu ya upendo wa Mungu imepungua katika mioyo yao, Lakini nguvu hii ya upendo ndio inawafanya watu wa Mungu nuru ya ulimwengu (EGW 1Selected Messages 357.1)

Je nguvu ya upendo kati ya mtu na mtu imepungua sana katika kanisa, Upendo wa kindugu umepungua sana. Lakini japokuwa upendo umepungua hivi bado tunajivunia kuwa tunajua kweli za neno la Mungu wakati upendo wa Mungu na haki yake haimo moyoni mwetu. Tunasema tunamjua Mungu wakati mioyo yetu ni migumu sana kumsaidia mwenye shida, Tunasema tunajua nuru za neno la Kristo wakati ukweli huo hatujauruhusu ufanye utakaso mioyoni kwetu. Tunapoyaona hayo yote jua kuwa Ujumbe wa kanisa la Laodekia unahusu hali zetu sisi kama waadventista wasabato. Uwepo wa Mungu haupo kati yetu.

Ujumbe kwa kanisa la Laodekia unahusu  waadventista wasabato ambao walikuwa na nuru kubwa na hawajatembea katika Nuru. Ni wale ambao walifanya taaluma kubwa, lakini hawakutunza hatua zao na kiongozi wao. Watatemwa watoke katika kinywa cha Mungu kama hawatatubu. (EGW, 2Selected Messages 66.2)

Ellen White amesema wazi kuwa ujumbe wa kanisa la Laodekia unahusu waadventista wasabato. Hili ni onyo la kila mmoja aliyendani ya kanisa la waadventista wasabato. Ndani ya kanisa la waadventista wasabato kuna wengi ambao wanajua ukweli  wenda wanaweza kuwa ni wachungaji, wazee wa kanisa, mashemasi, raisi wa General conference na viongozi wengine wengi na washiriki, lakini japokuwa wanajua ukweli huo, Hawaendi sawa sawa na Kweli hiyo, Yesu anasema kuwa waadventista hawa watatemwa watoke katika kinywa chake kama hawatabadili mienendo yao mibaya. Lakini Je watu hawa watatubu? kwa maana kanisa la Laodekia linaona ni tajiri na halina shida na kitu.

Hali ya kanisa inayowakilishwa na wale mabikira wapumbavu pia inaongelewa kama hali ya Laodekia. Shahidi wa Kweli anasema Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi (EGW, Review and Herald 19,1890)

Mtumishi wa Mungu Ellen White anasema kuwa wale mabirika watano wapumbavu ambao taa zao hazikuwa na mafuta ndio hali halisi ya kanisa la Laodekia. Kwa vile Ellen White anaona hali ya kanisa la waadventista wasabato inayofananishwa na wale mabikira watano ndio hali ile ile anayoiona katika kanisa la Laodekia, tunajua kuwa Kanisa la waadventista wasabato lisipofanya matengenezo litatapikwa litoke katika kinywa cha Yesu. Ellen White anazungumza na kanisa la waadventista wasabato akisema

"Tusifikirie kuwa tuna kweli zote, kwamba tunaelewa nguzo kuu za Imani yetu, na kutulia katika ufahamu huu, Ukweli ni ukweli endelevu lazima tutembee katika Nuru iliyoongezeka" (EGW, CW 33.2)

Mara nyingi sana kanisa linaamini kuwa lina nuru zote za Biblia na kutulia hapo, hili limekuwa ndio kiburi kikubwa cha kanisa la waadventista wasabato. Lakini Ellen White amesema wazi kuwa tusifikirie hata kidogo kuwa tuna Kweli zote,maana yake ni kwamba sio kweli kuwa tunakweli zote. Yoyote anayesema kuwa tuna kweli zote anaongea uongo na anafanya watu wasijisumbue kutafuta kweli katika biblia.  Amesema wazi kuwa kweli za Biblia huwa ni endelevu. Kanisa letu la waadventista wasabato kama jinsi lilivyo kanisa la Laodekia linadhania kuwa linakweli zote za Biblia na kuridhika jambo ambalo kwa maelezo ya Ellen White sio kweli. Sasa tuangalie ushauri wa Yesu kwa Kanisa la Laodekia ni nini?Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona. Yesu ameliambia Kanisa la Laodekia linunue kwake dhahabu iliyosafishwa kwa Moto, Lakini Dhahabu hii iliyosafishwa kwa moto maana yake ni nini? Ellen White anasema

"Dhahabu iliyotajwa na Kristo, shahidi wa kweli, ambayo wote tunatakiwa tuwenayo, imeoneshwa kwangu kwamba ni Kuwa katika Imani na upendo kwa ujumla, na upendo unaoweka mbele Imani"( 2T 36.2)
Tunaelewa kuwa Yesu aliposema kanisa la Laodekia linunue kwake Dhahabu iliyosafishwa maana yake ni kwamba kanisa la Laodekia lichukue kwake Imani na upendo ule ambao Yesu mwenyewe alikuwa nao. Ni kweli kuwa katika kanisa la Waadventista wasabato upendo umepoa sana kwahiyo Yesu analiambia kuwa linunue kwake upendo na Imani. Yesu pia analipa ushauri kanisa La laodekia kuwa linunue kwake mavazi meupe mavazi meupe yanayozungumziwa hapa ni haki ya Kristo. Kwahiyo Yesu anataka kanisa la Laodekia livae haki yake ili lisiwe uchi. Pia anazungumzia kuhusu dawa ya macho maana yake ni Kuwa na utambuzi wa mambo ya kiroho. Kwa maana nyingine ni kwamba Kanisa la Laodekia Halina haki ya Kristo, Halina Imani na upendo wala halina Utambuzi wa mambo ya kiroho. Sasa Je uwepo wa Mungu upo katika kanisa la Waadventista wasabato baada ya kuona kuwa limegeuka na kuwa Laodekia? Ellen White anasema

Kanisa lipo katika hali ya Laodekia. Uwepo wa Mungu haupo katikati yake. (EGW Last day Events, 49.1)
Japokuwa inawezekana ikawa ni Ngumu kuamini, lakini Ellen White amesema wazi kuwa uwepo wa Mungu haupotena na kanisa la waadventista wasabato kwasababu limegeuka na kuwa Kanisa la Laodekia

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA ALAMA YA MSALABA

MUNGU ANA NAFSI NGAPI?

1YOHANA 5:8 NA MATHAYO 28:19 ZINASEMAJE?