CHINI YA SHERIA.


Lakini Kabla ya kuja ile Imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria tumefungwa mpaka ije ile imani  itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa kristo ili tuhesabiwe haki kwa Imani. Lakini iwapo imani imekuja  hatupo tena chini ya  kiongozi. Kwakuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.”(Wagalatia 3:23-26).

Katika huu mstari kitu cha kwanza tunachoweza kujifunza ni kwamba kuja kwa ile Imani sio kuja kwa Kristo mwenyewe, maana huwa tunafikiri kuwa kuja kwa ile Imani  ndio kuja kwa Kristo mwenyewe hapa duniani . Mtume Paulo anasema kuwa “Kabla ya kuja ile Imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria” tunafanya kosa kutafsiri kuwa “kabla ya kuja kwa Kristo hapa duniani kwa mara ya kwanza tuliwekwa chini ya sheria”. Bali ni kabla ya Kuja kwa Imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, sasa swali la kujiuliza ni kwamba Imani inakujaje?

Basi Imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la kristo”(Warumi 10:17).
Imani inakuja kwa kusikia neno la Kristo, na neno la kristo ndilo kweli. Hivyo basi mtume Paulo anaposema kabla ya kuja ile Imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, maana yake ni kwamba kabla hatuja sikia habari njema za ukombozi na ukweli wa Neno la Kristo lioneshalo mapenzi ya Mungu, tulikuwa tumewekwa chini ya sheria. Imani inakuja pale ambapo tumesikia neno la kristo ambalo katika hilo tunafahamu Mungu wa Kweli ni yupi.. Kabla hatujasikia neno la Kristo tulikuwa gizani na vipofu, lakini Tuliposikia neno la Kristo basi Imani ikaja kwetu. Kipindi ambacho bado tulikuwa hatujasikia neno la Kristo tulikuwa chini ya sheria. Je kuwa chini ya sheria ni nini?

Lakini Mkiongozwa na Roho hampo chini ya sheria”(Wagalatia 5:18).
Maana yake ni kwamba kama Roho sio kiongozi wetu basi tupo chini ya sheria. Kwa hiyo kuwa chini ya sheria ni pale ambapo Roho haongozi matendo yetu na maisha yetu. Kuwa chini ya sheria ni kuongozwa na Roho wa Shetani. Hivyo wale wote walio chini ya sheria Roho wa Mungu sio kiongozi wao wapo katika matendo ya mwili

“Basi matendo ya mwili ni dhahiri ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo katika hayo nawaambia mapema kama nilivyokwisha kuwaambia ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu”(Wagalatia 5:20-21).
Sasa tunapata kufahamu nini? Kuwa kabla ya kusikia neno la Kristo Imani ilikuwa bado haijaja ndani ya Mioyo yetu, roho wa Mungu alikuwa sio Kiongozi wetu na tulikuwa tumefungwa katika hatia ya dhambi. Torati ilikuwa inatuhukumu kuwa sisi ni wadhambi na kifo ndio adhabu yetu. Katika kuona ubaya na hukumu ambazo Sheria inatushikilia tunaona tukimbilie kwa Kristo ili azifute hizo hukumu na hatia Sheria inazotushuhudia. Katika hilo basi Torati imekuwa kiongozi ili kutuleta kwa Kristo tuhesabiwe haki kwa Imani. Ile hukumu, ile hatia, ile adhabu ya kifo tuliyoipata baada ya kuvunja sheria inatufanya tukimbilie kwa Kristo ilituhesabiwe haki kwa imani, baada ya kuamini kuwa katika yeye ndipo ondoleo la dhambi linapatikana, Sasa Iwapo Imani imekuja hatupo tena chini ya kiongozi. Kuwa chini ya kiongozi ni kuwa chini ya sheria. Tunatambua kuwa baada ya kusikia neno la kristo liletalo uzima, na kuamini juu ya ahadi zilizopo ndani ya Kristo ikiwamo ahadi ya Msamaha wa dhambi, basi Roho wa Mungu anakuwa ni kiongozi wa matendo yetu na pia kiongozi wa maisha yetu. Sheria haituhukumu kuwa ni wavunjaji wa sheria tena kwa maana hatupo tena chini ya sheria bali tupo katika sheria, tunakuwa tena sio wavunjaji wa sheria, bali watiifu wa sheria. Maana kila aliyechini ya Sheria au chini ya kiongozi ni Mvunjaji wa sheria. Baada ya Imani kuja ndani ya mioyo yetu sisi sio tena wavunjaji wa Sheria bali wafataji na watiifu wa sheria ya Mungu. Katika hili tumekuwa wana wa Mungu kwa njia ya Imani kwa Yesu Kristo. Na kama sisi ni Wana wa Mungu kupitia Kristo, basi tumekuwa uzao wa Ibrahimu.

Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu hamwi chini ya sheria  bali chini ya neema”(Warumi 6:14).

Katika huu mstari unaoendelea kufafanua wazi nini maana ya kuwa chini ya sheria, walio chini ya neema dhambi haina nguvu tena kwao kwa maana Roho wa Mungu anakaa ndani yao. Bali walio chini ya sheria dhambi ndio inawatawala kwa maana roho wa shetani anakaa ndani yao. Tunaendelea kujua kuwa, kuwa chini ya sheria ni kutawaliwa na dhambi na roho wa Mungu sio Kiongozi wa watu hao. Bali roho wa Mungu ni kiongozi wa wote walio chini ya neema yaani walio katika utii wa Sheria za Mungu. Msomaji asisahau kanuni hii ya kwamba, kuwa chini ya sheria SIO KUTII AU KUFATA SHERIA, BALI NI KUVUNJA AU KUTOKUTII SHERIA YA MUNGU. WALIO CHINI YA SHERIA ROHO WA MUNGU SIO KIONGOZI WA MATENDO YAO BALI NI ROHO WA SHETANI. Walio chini ya sheria ni wavunjaji wa Sheria. Kristo amekuja kutukomboa sio katika kutiii sheria bali katika kuvunja sheria. Yoyote aliyechini ya sheria ni mvunjaji wa sheria na mvunjaji wa sheria anakuwa katika laana ya sheria.

 Na alaaniwe asiyeyaweka imara maneno ya torati hii kwa kuyafanya. Na watu wote waseme, Amina. (Kumb. 27:26)
Yesu alikuja kututoa katika laana ya sheria, na kutuokoa tutoke kuwa chini ya sheria. Kwa kutupa Roho wake atuongoze, Yesu alitukomboa tusiwe chini ya sheria. Kwa maana kuwa chini ya sheria ni kuwa katika ya laana ya torati iliyokuja baada ya kuvunja Sheria za Mungu.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA ALAMA YA MSALABA

MUNGU ANA NAFSI NGAPI?

1YOHANA 5:8 NA MATHAYO 28:19 ZINASEMAJE?